MARA
nyingi vijana hupata taabu sana katika suala la kuchagua mchumba.
Vijana wa kiume ndio hasa hupata wakati mgumu zaidi kwani jamii imewapa
wajibu wa kuanzisha mazungumzo yahusianayo na mapenzi.
Hata
hivyo, vijana wa kike nao wanao wajibu wa kuchagua ili kuhakikisha kuwa
hawaanguki mikononi mwa mabazazi wa kuwalaghai na kuwatumia kwa raha za
miili yao kisha kuwaacha kwenye mataa.Ni jambo la kawaida kwa vijana
walio wengi, wawe wa kike au wa kiume, kuangalia sura na mwonekano wa
mtu.
Lakini
unapotafuta mchum ba kwa malengo ya kuishi naye maisha yako yote kama
mume na mke haipendezi kuangalia tu mwonekano, maana Waswahili husema si
kila king’aacho ni almasi. Kwa sababu hiyo, hapa yatabainishwa mambo
muhimu ya kuangalia na kuzingatia katika suala hili.
1. UADILIFU
Pamoja na sifa zote za uzuri zinazoweza kubainishwa na kufanywa kuwa
vigezo vya uzuri wa mwanamke na mwanaume na hata zikatumiwa kumpata Miss
au Mr Tanzania, sifa kuu impasayo mtu anayefaa kuwa mchumba kuwa nayo
ni sifa ya uadilifu.
Mtu
anapokuwa na uadilifu (pengine uaminifu), maana yake ni kwamba tabia ya
mtu huyu anayoionesha nje ndiyo tabia yake halisi na anapofanya jambo
jema analifanya kwa roho yake na si kwa unafiki.Mtu anapokuwa mwadilifu
ataheshimu maadili na kufanya wema, hata pale inapokuwa rahisi kwa
wengine kukengeuka na kufuata njia za mkato ambazo mara nyingi si za
halali.Mtu mwadilifu pia huwa na sifa za ukweli na kujitolea kuwasaidia
watu wengine bila kujali faida – haya yote ni mambo muhimu ambayo mtu
mwenye kuwa nayo huwa na msingi wa ujenzi wa uhusiano imara na wa
kudumu.Watu wanaoweza kujivunia furaha ya kweli katika maisha yao ya
ndoa, ni watu ambao wamekutana wote wakiwa na sifa ya uadilifu ambayo
hujumuisha mambo mengi.
Zipo
ndoa nyingi zenye furaha ya bandia. Furaha hii mara nyingi hutokana na
ridhiko la kimwili alipatalo mtu kutokana na kukidhiwa kwa mahitaji yake
ya kimwili yanayohusiana na haki za msingi za binadamu – yaani chakula,
mavazi na malazi. Lakini furaha ya kweli ya maisha ya ndoa, watu
hawaipati isipokuwa katika uhusiano ambao wenza wamethibitishana kuwa
waadilifu.
2. HEKIMA,
Mtu mwenye uadilifu wa kweli, mbali na kuwa mwema kwa mwenzake, pia
huhakikisha anakabiliana kwa busara na hekima na matatizo yote
yanayoweza kusababisha kuyumba kwa uhusiano, hususan yale yaliyo nje ya
uwezo wake.Uzoefu unaonesha kuwa wapenzi, hususan wanandoa walio katika
uhusiano wa muda mrefu wanaoendelea kufurahia unyumba wao si wale ambao
walipendana kwa mvuto na wala hawana mambo mengi ya asili
yanayowaunganisha kuliko wale wanaotengana.
Lakini
la muhimu ni kwamba watu hawa huwa wamejifunza jinsi ya kukabiliana kwa
hekima na matatizo yanayojitokeza, hususan yale yanayotokana na tofauti
zao kimtazamo.Ukiachilia mbali sifa ya uadilifu, watu hawa huwa
wamejifunza kukabiliana na matatizo kuhusiana na uzazi na ulezi wa
watoto, uhusiano na ndugu, jamaa na marafiki, suala la ngono, fedha na
maisha ya unyumba kwa ujumla.Habari njema ni kwamba uadilifu na hekima
ni mambo ambayo mtu yeyote anaweza kujifunza na kisha kufanyia kazi.
Ndiyo
maana wanandoa hufundishwa kabla ya ndoa na hata wanapokuwa tayari
wameoana huendelea kuhudhuria semina za kidini na kijamii kwa ajili ya
kujiimarisha.Kwa hiyo, kama mume/mke wako mtarajiwa anaonekana kuwa na
utayari wa kujifunza kuhusiana na jinsi ya kuishi na mtu wa jinsia
nyingine, ana nafasi kubwa ya kuwa mke/mume mzuri baadaye.
3. UPOLE,
Mfalme Suleiman katika mojawapo ya semi zake za hekima alisema mwanamke
mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake. Yamkini ndivyo ilivyo
pia kwa mwanaume mpumbavu, maana upumbavu haujengi.Siku zote kitu
kinachovunja uhusiano wa kindoa si makombora ya nyuklia, bali ni ulimi.
Kwa kadri mtu anavyoutumia ulimi wake anaweza kuijenga au kuibomoa
nyumba yake.Katika kumwangalia mtu ambaye unaweza kujenga naye nyumba ya
kudumu, ni vema kumchunguza na kuhakikisha kuwa si mtu mwenye kupenda
kurefusha maneno, maana hakika huyu atasababisha ugomvi mara kwa mara na
uhusiano hautadumu.
Wapo
watu ambao ndoa zao zina sifa ya ugomvi na karibu kila mtu anafahamu na
hata wamekuwa kero kwa ndugu, jamaa na majirani zao, mara kwa mara
wakiwaamsha watu usiku wa manane wakitafuta suluhu.Mara nyingi wanaume
ndio huanzisha ugomvi, lakini ugomvi huwa na nguvu zaidi kama mwanamke
ni msemaji. Dawa ya kuzuia ugomvi usiokuwa na mpango ni kupunguza maneno
na kuepuka kutafuta ushindi katika ubishi. Lakini kinga ya tatizo hili
ni kuepuka kujiingiza katika uhusiano na mtu ambaye umejihakikishia kuwa
si mwingi wa maneno.
Bahati
nzuri, jamii huwatambua wanawake/wanaume ambao wanaweza kuwa wake/waume
bora baadaye kwa hiyo ni wajibu wa mtafutaji kuhakikisha kuwa anafanya
uchunguzi wa kina kabla ya kujitosa kwa mtu ambaye baadaye
atamtaabisha.Mwanandoa aliyeifahamu vema dhana ya ndoa – kwamba ni
maisha ya kuvumiliana na kuchukuliana, hufahamu ni wakati gani wa kusema
na wakati gani wa kukaa kimya.
Mtu
huyu pia hufahamu njia nzuri na salama ya kujiondoa kwenye tatizo
anapoona mwenzake anaelekea kubaya, ili hatimaye uhusiano wao uendelee
kuwa salama japo wao wanaweza kuwa wamekwaruzana.Mtu huyu mwenye upole
hujiweka katika mkao wa upatanishi na huhakikisha kuwa kila mjadala
mkali unapita na kumalizika salama. Ni wazi kuwa katika kutafuta, kama
hukukurupuka, utamwona mtu mwenye hulka hii – upole.
4. MVUTO,
Hisia za mvuto wa kimapenzi ni muhimu katika kujenga uhusiano. Mtu
mmoja akauliza, ni yupi bora – yule anayenivutia sana au yule
anayenipenda sana? Maisha ni ya ajabu sana. Huwa inatokea kuwa mtu
unayevutiwa naye sana yeye havutiwi nawe, bali anavutiwa na mwingine
ambaye naye hana mpango naye!Haya ndiyo maisha. Uzoefu unaonesha kuwa
asilimia kubwa ya watu walio katika ndoa hawajawaoa/kuolewa na watu
waliokuwa wakiwapenda sana enzi za ujana wao, au wale waliotimiza ndoto
za ujana wao. Bahati njema miongoni mwa wanandoa hawa wapo wale wenye
ndoa imara sana.
Mvuto
wa kimapenzi ni muhimu sana, lakini watu husema maji yakisema usininywe
yajibu kuwa wewe pia huna kiu nayo. Japo inaweza kuonekana kama ni aina
ya ‘sizitaki mbichi hizi’ lakini si vema kujisumbua na mtu
asiyekupenda.Badala ya kujihangaisha na mtu asiyekupenda, kaa chini na
umsubiri anayekupenda hata kama huhisi kuvutiwa naye sana.
Baadaye
utamzoea na maisha yatakuwa mazuri, kisha utajiuliza baadaye yule
aliyekuringia alikuwa na nini cha ziada?Lakini iwapo mambo mengine yote
yatakwenda sawa, ni vema na muhimu kabisa kuhakikisha kuwa mtu
unayepanga kuwa naye maisha yako yote ni mtu anayekuvutia kimwili na
kiakili, maana vinginevyo unaweza kupata sababu ya kukidhi kiu yako nje –
jambo ambalo si maadili mema katika ndoa na maisha.NI MUHIMU KUWA
MAKINIKatika nyakati za ujana, watu wengi hubabaishwa kwa mengi.
Vijana
wa kiume hubabaishwa na sura, maumbile na pengine rangi na kusahau
mambo muhimu yaundayo orodha ya sifa za mke mwema.Kwa upande wao, vijana
wa kile pia waweza kubabaishwa na pesa, maumbile, sura, utanashati,
umaarufu au kuchoshwa na shinikizo la umri, hivyo kujikuta
wakijitumbukiza kwa wanaume wasio na sifa za waume wazuri.Lakini
tukirejea kwenye msemo wa zamani kuwa uzuri si hoja bora tabia, ni wazi
kuwa tutafikia mahali tutajenga mahusiano imara na yasiyotikiswa na
sunami zozote za kimaisha. Ilimradi tu uhakikishe kuwa mtu mwenyewe
anakupa mvuto kimapenzi, maana vinginevyo kutakuwa hakuna maana.
Facebook Blogger Plugin by Michapo Blog
Post a Comment