Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu 17 wakiwemo waganga wa jadi 10 wakihusishwa na tukio la kikatili katika kijijini cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ambako mtoto mlemavu wa ngozi (albino), Baraka Cosmas (6) mwishoni mwa wiki alishambuliwa na kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana.
 
Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni watu saba ambao wanatuhumiwa kushiriki katika kumkata kiganja mtoto huyo mlemavu wa ngozi akiwemo baba yake mzazi, Cosmas Yoram (32).
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Ferdinand Rwegasira amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao kufuatia msako mkali uliofanyika katika vijiji vinne vya wilaya za Sumbawanga na Nkasi.
 
Aliwataja waliokamatwa pamoja na baba mzazi wa mtoto huyo kuwa ni pamoja na Mwendesha William (30), Masunga Bakari (50), na Ngolo Masingija (47) wote kutoka kijiji cha Kaoze .
 
Wengine ni Paschal Jason (40), David Kiyenze (45) na Mageta Shimba (46), wote wakazi wa kikiji cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.
 
Kwa mujibu wa Rwegasira, katika msako huo pia walikamatwa waganga wapiga ramli chonganishi 10 akiwemo Sererino Kachingwe “Nakalango”(70), mkazi wa kijiji cha Miangalua wilayani humo ambaye pia alipatikana na bunduki aina ya Shot gun greener yenye namba G 73354 TZD,CAR 47478 ambayo anaimiliki isivyo halali .
 
“Mtuhumiwa huyu pia ni mganga wa kienyeji ambapo alikutwa na wanyama wawili aina ya Kalunguyeye wakiwa hai pamoja na dawa mbalimbali za miti shamba.
 
"Pia katika msako huo amekamatwa mganga mwingine wa kienyeji , Eliza Malongo mwenye umri wa miaka 36 mkazi wa kijiji cha Kamnyalila akiwa na nyara za Serikali, “ alieleza.
 
Aliongeza Eliza alikutwa na ngozi ya chui, wanyama wanne waliokaushwa aina ya Kalunguyeye na nywele zinazodhaniwa kuwa za binadamu pamoja na mfupa wa swala.
 
Waganga wengine waliokamatwa katika msako huo ni pamoja na Sodeli Malimbo ‘Chuchi” (69) mkazi wa kijiji cha Miangalua, Akobo Chinzwe (50), Leonard Samson (59) na Engelbert Kasinde (45) , wote wakazi wa kijiji cha Kamyalila.
 
Katika orodha hiyo wapo Boniface halya (49) na Julius Simbamwene (40) wote wakiwa wakazi wa kijiji cha Mpui .
 
“Watuhumiwa hawa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kupigia ramli vikiwemo vioo viwili, pembe moja, ndege na wanyama ambao hawakuweza kutambulika mara moja, mizizi ya aina mbalimbali na dawa mbalimbali za kienyeji,“ alieleza Rwegasira.
 
Akifafanua zaidi, Rwegasira alidai kuwa msako huo pia ulifanyika wilayani Nkasi ambako alitiwa nguvuni mganga wa kienyeji aitwae Charles Misalaba (47) , mkazi wa kijiji cha Kacheche ambapo alikutwa na yai la mbuni , kucha za chui , pembe ya korongo , ngozi ya paka pori na kobe aliyekaushwa.
 
Amesisitiza kuwa msako huo bado unaendelea na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara tu baada ya upelelezi wa awali wa shauri lao kukamilika.
 
Kwa mujibu wake msako huo unafuatia watu wasiojulikana kumshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kisha kutokomea nacho kusikojulikana usiku wa kuamkia Machi 08, mwaka huu.
 
Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban pamoja na watoto wengine wawili ambao nao ni albino wakiwa na umri wa miaka nane na minne.
 
Alisema tukio hilo ni la saa nane usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo.
 
Akielezea zaidi, Kaimu Kamanda Rwegasira alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
 
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya …
 
“Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojulikana,” alibainisha.

Shiriki nasi kwa kutoa maoni yako hapa chini

Facebook Blogger Plugin by Michapo Blog

Post a Comment

 
Top