LICHA ya Serikali, jamii na jumuiya ya kimataifa kukemea ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), bado kuna wanaoendelea kung’ang’ania mila potofu za kuamini kwamba bila ya ushirikina unaohusishwa na matumizi ya viungo vya albino, hawawezi kufanikiwa kimaisha, iwe katika kisiasa au kibiashara.

Hayo yanathibitishwa na kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya ukatili dhidi ya albino, ambapo usiku wa kuamkia jana, watu wasiojulikana walimshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kisha kutokomea nacho kusikojulikana.

Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda.

Alisema tukio hilo ni la saa 8 usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo.

Akielezea zaidi, Kamanda Mwaruanda alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
  
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya … 
  
“Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana,” alibainisha.

Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.

Kwa mujibu wa Mwaruanda, mtoto huyo amelazwa katika katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama yake mzazi.

“Watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo hicho cha kiganja cha mkono wa mtoto Baraka,” alisisitiza Kamanda.

Shiriki nasi kwa kutoa maoni yako hapa chini

Facebook Blogger Plugin by Michapo Blog

Post a Comment

 
Top